Historia ya wekundu wa msimbazi simba sports club
Simba SC ni moja kati ya timu nne kongwe kabisa hapa nchini ikianzishwa mwaka 1936 jijini Dar es salaam. Zingine ni vinara Yanga SC 1935, African Sports 1936 na Coastal Union 1938.
Simba imepitia majina mengi toka kuanzishwa kwake mpaka sasa. Ilipoanzishwa mwaka 1936 iliitwa Queens jina lilidumu mpaka mwaka 1948 walipofanikiwa kupanda ligi daraja la kwanza na wakati huo mkoa wa Pwani ulianzisha ligi maalumu iliyokuwa ikijiendesha kwa misingi bora ya kisasa.
Wakati huu ndio Simba ilianza kupata ufadhili unaoeleweka mfano jezi nzuri za kisasa na viatu wakati wenzao wakiwa bado wakilisakata kabumbu peku peku .
Simba walibadilishwa jina na kuitwa Eagles baada ya kuonekana jina la Queens linawaletea kebehi kwa watani wao wa jadi Yanga SC ambao kabla ya mwaka 1930 walijulikana ‘ New Young ‘.
Jina la Eagles yaani tai kwa lugha ya kiswahili halikudumu sana. Lilikaa kwa muda mchache sana na kubadilishwa kuwa Sunderland.
Hili ndio jina ambalo wengi wanalifahamu sana . Ni jina ambalo wekundu hawa wa msimbazi wana kumbukumbu nalo kubwa na ndefu kidogo.
Baada ya nchi kupata Uhuru mwaka 1961 na miaka minne baadae kuanzishwa ligi daraja la kwanza yenye sura ya kitaifa yaani ligi iliyoshirikisha timu zote za bara na visiwani, Sunderland ndio ilikuwa timu ya kwanza kubeba kombe la ligi hiyo mwaka 1965 na kulitetea tena kombe hilo mwaka 1966.
Hivyo katika historia Simba SC wakitumia jina la Sunderland waliweza kunyakua ubingwa wa ligi daraja la kwanza mara mbili kabla ya jina hilo kufa mwaka 1971 baada ya raisi wa kwanza wa Zanzibar hayati Abeid Karume kuwashauri kubadili jina kwa sababu ya maudhui yake kikoloni na ndipo jina la Simba SC lilipozaliwa.
Sunderland wakitumia jina jipya la Simba SC iliwachukua miaka miwili kujipanga kurudisha makali yao katika ligi. Mwaka 1973 walitwaa tena ubingwa wa ligi daraja la kwanza ingawa waliporwa tena na Yanga 1974. Hivyo kihistoria Simba hii mpya ilitwaa ubingwa wa ligi kwa mara ya kwanza mwaka 1973 na mara ya mwisho mwaka 2012.
Miaka ya 60 na 70 Simba walikuwa imara sana kwenye scouting ya wachezaji. Timu nyingi Dar es salaam zilitegemea matawi ya Simba ambayo yalikuwa yakitumika kulea vipaje wakiwemo Simba wenyewe.
Matawi maarufu wakati huo kama Morning Stars, Ilala Stuffs, Canada dry na Liverpool . Yalikuwa matawi ya Simba pia timu maarufu wakati huo za kulea vijana kama walivyo Bom bom hivi sasa. Wachezaji mahiri na waliokomaa vyema walikwenda Simba kwanza na wengine kwa vilabu vingine lakini sio Yanga.
Historia ya mwisho kwa mnyama huyu kwa miaka hiyo ni mwaka 1976. Huu mwaka Simba waliitwa mashujaa wa jiji la Dar es salaam kisoka baada ya kulilejesha kombe la ligi daraja la kwanza baada kwa mara ya kwanza mwaka 1975 kombe hilo kuchukuliwa na timu ya mkoani yaani wababe wa mji kasoro bahari Mseto.
Wakati huu ndio Simba walikuwa na wakali wake kama King Kibadeni . Kipindi hiki ndipo Simba walijiwekea historia yao ya kubeba ubingwa wa ligi mara tano mfululizo 1976, 1977, 1978, 1979 na 1980.
Baada ya hapo mnyama alipotea msituni hadi aliporudi tena kwenye ubingwa mwaka 1984.
Huyo ndio mnyama Simba SC kwa ufupi kuanzia mwaka 1936 mpaka 1980.
Leave a Comment